Na Raymond
Mihayo
Kahama
March 25, 2014.
HALMASHAURI YA USHETU NA MSALALA WAVUTANA KUHUSU MRAHABA WA BULYANHULU.
HALMASHAURI mpya za Msalala na Ushetu Wilayani
Kahama Mkoani Shinyanga juzi zimevutana kuhusu fedha za mapunjo zilizotolewa na
Mgodi wa Bulyanhulu pamoja na Ushuru wa zao la Tumbaku kufuatia Halmashauri
iliyokuwa mama ya Wilaya ya Kahama kufa na kuzaliwa kwa Halamsahuri hizo.
Katika kikao cha dharura cha Baraza la Madiwani wa
Halmashauri ya Msalala kilichohudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Kahama Benson
Mpesya na Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga Anselim Tarimo ilishuhudia
Madiwani hao wakigoma kutoa kiwango cha shilingi milioni 610 katika shilingi
bilioni 1.4 zilizotolewa na Mgodi wa Bulyanhulu kama mapunjo.
Mgodi huo wa Dhahabu wa Bulyanhulu ulitoa kiasi
hicho cha fedha kwa malengo ya kugawana nusu kwa nusu fedha hizo baada ya ile
iliyokuwa Halmashauri ya Wilaya ya Kahama kufa na kuzaa Halmashauri hizo mbili
za Ushetu na Msalala.
Akisoma taarifa ya mrejesho wa Mgawanyo wa fedha
hizo za mapato ya ndani kutoka katika Mgodi wa African Barrick Gold Bulyanhulu
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Msalala Patrick Karangwa alisema kuwa katika kikao
cha kamati ya fedha kilichokaa tarehe 27/1/2014 walijadili taarifa ya fedha
hizo na kufikia maagizo.
Alisema baadhi ya maagizo walifikia ni Mkurugenzi wa
Halmashauri ya Ushetu kufuatilia malipo ya Ushuru ya zao la Tumbaku kwa mwaka
2012/2013 wa iliyokuwa Halmashauri ya Wilaya ya Kahama ambao pia unastahili kugawanywa
kwa Halmashauri zote mbili za Ushetu na Masalala.
Hata hivyo Karangwa alisema kuwa baada ya
ufuatiliaji uligundua kuwa mapato ya Ushuru wa zao oa Tumbaku kwa mwaka huo ulikuwa ni kiasi cha shilingi
milioni 738.6 ambapo fedha hizo zilitakiwa kugawanywa kwa Halmashauri zote
mbili.
Alisema Tarehe 05/2/2014 Halmashauri ya Wilaya ya
Msalala ilihamisha kiasi cha fedha cha shilingi milioni 240.6 kwenda Halmashuri
ya Ushetu baada ya kutoa mgawanyo wa
mapato ya tumbaku kutoka katika mgawo wa shilingi milioni 610 kwenye fedha
kutoka Barrick Bulyanhulu.
Hata hivyo Halmashauri ya Wilaya ushetu ilikataa
fedha hizo na hivyo kuzuia fedha za matumizi kutoka serikali kwenda Halmashauri
ya Msalala ili kufidia fedha zilizokatwa hali ambayo ilizua mgogoro mkubwa
baina ya Walimu na Mkurugenzi wa Ushetu Isabela Chilumba.
Hata hivyo katika kikao hicho kilichodumu kwa muda
wa masaa sita kiliisha baada makubaliano chini ya Mkuu wa Wilaya Benson Mpesya
na Katibu tawala Mkoa wa Shinyanga Anselim Tarimo kuunda tume kwa ajili kufuatilia
fedha hizo pamoja na nyingine zilizopaswa kugawanywa baada ya iliyokuwa
Halmashauri ya Wilaya Kahama kufa na kuzaa Halmashauri hizo.
mwisho
No comments:
Post a Comment